Search This Blog

Tuesday, November 9, 2010

HALMASHAURI NANE KUONGOZWA NA UPINZANI


Halmashauri nane nchini zitaongozwa na vyama vya upinzani baada ya kupata viti vingi vya udiwani katika Uchaguzi Mkuu wa wiki iliyopita.
Halmashauri hizo ni Karatu, Manispaa ya Moshi, Kigoma Mjini, Moshi Vijijini, Ukerewe, Jiji la Mwanza, Kasulu na Mbulu.
MWANZA
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kitaliongoza Jiji la Mwanza linaloundwa na majimbo ya Ilemela na Nyamagana kufuatia kushinda kata 11 dhidi ya kata nane zilizochukuliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Uchaguzi katika kata za Mirongo na Mkuyuni uliahirishwa hadi baadaye. Hata hivyo, matokeo yake hayawezi kusababisha athari yoyote kwa kuwa hata kama CCM itashinda itakuwa na viti 10 na isitoshe kata hizo inasemekana ni ngome za Chadema.
KARATU
Katika matokeo ya udiwani Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilishinda halmashauri ya Karatu kwa kupata kata 10 na kata nne kuchukuliwa na Chama Cha mapinduzi (CCM).
UKEREWE
Katika Jimbo la Ukerewe, Chadema imefanikiwa kupata viti 13 kati ya 24 vya udiwani hali inayokiwezesha kuongoza halmashauri hiyo, CCM imepata viti 10 huku CUF ikiwa na kiti kimoja.
KiGOMA MJINI
Chadema imeshinda katika kata 10 wakati CCM imeshinda katika kata tisa.
JIMBO LA MOSHI MJINI
Chadema italiongoza jimbo la Moshi Mjini baada ya kupata kata 17 kati ya kata 21. CCM imepata kata nne.
MOSHI VIJIJINI
Halmashauri ya Moshi Vijijini inayoundwa na majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo, itaongozwa na Chadema kwa kushirikiana na TLP baada ya kupata viti 16 dhidi ya 15 za CCM.
Katika Jimbo la Moshi Vijijini CCM ilipata kata tisa, Chadema kata saba na TLP sifuri wakati katika Jimbo la Vunjo TLP ilipata kata saba, Chadema kata mbili na CCM kata sita.
KASULU
Halmashauri ya Kasulu pia imekwenda kwa upinzani uliopata madiwani 14 dhidi ya madiwani 11 wa CCM. Halmashauri hiyo itaongozwa kwa pamoja kati ya Chadema kilichopata viti madiwani wane na NCCR-Mageuzi kilichopata madiwani 10.
MBULU
Halmashauri ya Mbulu itaongozwa na Chadema baada ya kushinda kata 17 dhidi ya kata 15 zilizochukuliwa na CCM.
ARUSHA
Hata hivyo, katika Jimbo la Arusha Mjini huenda likaongozwa kwa mseto baada ya Chadema kupata madiwani 8, TLP 1 na CCM 10. Kwa kuwa Chadema kilishinda ubunge na mbunge ni sehemu ya madiwani, hivyo chama hicho na TLP vitakuwa na madiwani 10 sawa na CCM hivyo kuongoza kwa mseto.
Hata hivyo, idadi ya madiwani wa viti maalum inaweza kuamua ni chama kipi kiongoze halmashauri hiyo. Chadema kimepata madiwani 8, TLP 1 na CCM 10.

No comments:

Post a Comment