Search This Blog

Tuesday, February 15, 2011

BARAZA LA MAWAZILI KIVULI HILI HAPA

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe jana alitangaza Baraza la Mawaziri Kivuli likiwa na mawaziri 29 wote kutoka Chadema. Katika Baraza hilo, Mbowe amewateua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kuwa Waziri Kivuli wa Fedha, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika kuwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kuwa Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Kwa upande wa Mdee, atakuwa ana kwa ana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye alianza kutekeleza wajibu wake katika wizara hiyo kwa kasi baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete.

Mbowe akitangaza Baraza lake Kivuli jana alisema, anaweza kulifanyia mabadiliko na kuhusisha wabunge wa
vyama vingine vya upinzani wakati wowote na kwamba mabadiliko yatafanyika baada ya wao (wapinzani) kuzungumza na kufikia muafaka. Katika baraza hilo lililotangazwa baada kipindi cha maswali na majibu, Mbowe mwenyewe anakuwa Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi huku naibu wake akiwa Silinde David Ernest.

Idadi ya Mawaziri Kivuli
Mbowe alisema baraza lake halina mawaziri wengi ili kuonyesha mfano wa kukwepa matumizi yasiyokuwa ya lazima kwa vitendo."Pamoja na idadi ya mawaziri na naibu mawaziri wa Serikali kuwa 50, uteuzi wangu umeteua wasemaji wakuu na manaibu wasiozidi 29 ili kuonyesha kwa kivitendo, kilio chetu cha muda mrefu cha kuwa na baraza dogo la mawaziri.

Mawaziri wengine kivuli
Kwa mujibu wa Mbowe, Waziri Kivuli katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), amekuwa Raya Ibrahim Khamis, Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji amekuwa Esther Matiko huku naibu wake akiwa Vicent Nyerere.

Mbowe alimteua Said Amour Arfi kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora, Mchungaji Israel Natse kuwa Waziri wa Mahusiano na Uratibu, huku Susan Lyimo akiteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Pauline Gekul ameteuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Leticia Nyerere Waziri wa Ofisi hiyo akishughulikia mazingira ambapo Zitto Kabwe amekuwa Waziri wa Fedha huku naibu wake akiwa Christina Mughwai.

Godbless Lema amekuwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Tundu Lissu, Katiba na Sheria, Ezekia Wenje akienda Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Joseph Selasini alipewa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Silvester Kasulumbai akiteuliwa kuongoza Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Wengine walioteuliwa na wizara zao katika mabano ni Profesa Kulikoyela Kahigi (Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Halima Mdee (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi) na Mchungaji Peter Msigwa (Maliasili na Utalii).

Mhandisi Salvatory Machemuli ataongoza Wizara ya Ujenzi, Mhonga Ruhwanya (Wizara ya Uchukuzi), Lucy Owenya (Viwanda na Biashara), Christowaja Mtinda (Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk Gervas Mbasa (Afya na Ustawi wa Jamii).

Pia wamo Regia Mtema (Kazi na Ajira), Naomi Kaihula (Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto), Joseph Mbilinyi (Habari,Vijana na Michezo), Mustapha Akunaay (Ushirikiano wa Afrika Mashariki), Meshack Opulukwa (Kilimo, Chakula na Ushirika) na Highness Kiwia amekuwa Waziri Kivuli wa Maji.  

No comments:

Post a Comment