Search This Blog

Monday, February 7, 2011

MATUMIZI YA MAJINA YA VIONGOZI NA WANASIASA KATIKA MASHULE YA SERIKALI NA BINAFSI LINI MWISHO WAKE?

Matumizi ya majina ya wanasiasa na viongozi kwenye mashule na taasisi mbalimbali yalianza kuwa makubwa pale Serikali ilipoanzisha kampeni kubwa ya ujenzi wa shule za sekondari ili ziweze kuchukua ongezeko kubwa la wanafunzi waliotarajiwa kuingia kidato cha kwanza. Wanasiasa na Viongozi waliona hapo ndipo mahali pa kuchukulia ujiko. Baadhi yao walishinikiza zipewe majina yao. Hata watu waliokuwa hawajatoa mchango wowote wa maana kwa jamii, walitaka shule ziitwe kwa majina yao. Ilikuwa rahisi kwao kudandia sifa kwenye shule kuliko zahanati, hospitali au barabara zilizojengwa kwa nguvu ya wananchi.

Matokeo yanaonyesha wanafunzi waliomaliza fomu four hawakufanya bidii kusoma na kupata alama nzuri kulingana na sifa za wenye majina ya shule wanazosoma. Au labda tuamini kuwa majina yaliyotumika pia yalichangia kufeli kwa wanafunzi???? Tafakari.
Shule ya Yusuf Makamba Dar es Salaam ina rekodi  ya DI=2, DII=4, DIII=19, DIV=113 na waliofeli 314; Shule ya Pius Msekwa (Mwanza) imetoa DI=1, DII=2, DIII=9, DIV=60 na waliofeli 58.  Ali Hassan Mwinyi (Tabora) DI=0, DII=3, DIII=2, DIV=38 na waliofeli 67. Cyril Chami (Kilimanjaro) DI=0, DII=0, DIII=1, DIV=22 na waliofeli 54; Mengine jaribu kuangalia NECTA. 

Viongozi ambao majina yao yametumika kwa heshima na kumbukumbu ya kazi waliyofanya, au kwa kushinikiza kwao waone wajibu wa kutoa ushauri na kusukuma mbele maendeleo ya elimu. Pia wanapaswa kuwa walezi wa shule husika.Wanasiasa hao wanapaswa kusaidia kutatua matatizo yanayokabili shule hizo ili ziwe na mazingira mazuri ya kuleta matokeo bora kila mwaka kulingana na heshima ya majina yao katika jamii.

Lakini kama hakutakuwepo na nia njema ya kuangalia maendeleo ya shule zetu ambazo zina majina ya viongozi basi SIFA hii ya kushinikiza matumizi ya majina ya viongozi na wanasiasa haitaishia hapo, itafikia hatua hata makanisa na misikiti yataitwa kwa majina yao. Usije shangaa ukaja kusikia Alli Hassan Mwinyi SDA Church, au Msikiti wa Edward Lowasa, sehemu nyingine utaweza kusikia Salima Kikwete Full Gospel Fellowship Church. 

Tunachoomba si kutoa tu majina bali kuangalia namna gani ya kuinua maendeleo ya jamii ili kuleta maisha bora kwa jamii husika. Kitu kingine hivi tabia hii ya kuita taasisi kama shule majina ya watu hata wengine ambao hawajatoa mchango wowote katika jamii itaisha lini???. Maana kila siku kuna viongozi na wanasiasa wapya wanaibuka na kila mtu atataka jina lake litumike kwenye shule ama taasisi fulani ili tu ajipatie ujiko!!!!
Nawasilisha!!!!!

No comments:

Post a Comment