Noti za zamani bado ni fedha halali na zina thamani sawa na zile mpya. Zitaendelea kutumika na kuwepo katika mzunguko sambamba na hili toleo jipya la noti mpaka hapo hizo za zamani zitakapotoweka taratibu na hatimaye kwisha kabisa kwenye mzunguko. Hivyo basi, wananchi wanashauriwa kuendelea kuzipokea na kuzitumia noti za zamani bila shaka au wasiwasi wowote kuhusu uhalali wake hadi hapo zitakapokwisha na kutoweka kabisa katika mzunguko. Vilevile ieleweke kuwa hakutakuwa na ubadilishaji wa kupeleka noti za zamani benki na kutaka kupewa mpya.
Toleo hili la noti mpya lina taswira inayozingatia mandeleo ya uchumi na jamii. Tumefanya mabadiliko kidogo katika toleo jipya kwa kuweka picha za waasisi wa taifa letu. Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anaonekana kwenye noti ya shilingi elfu moja na Hayati Sheikh Abeid Amani Karume kwenye noti ya shilingi mia tano. Noti tatu zilizosalia yaani elfu mbili, elfu tano na elfu kumi zitaendelea kuwa na picha za wanyama pori ambao wanapatikana kwa wingi kwenye hifadhi na mbuga zetu za wanyama. Hata hivyo, kutokana na kupunguza ukubwa wa noti hizi mpya tumeweka picha za vichwa vya wanyama hao badala ya wanyama wazima kama ilivyo kwenye noti za zamani.
Ili kupambana na uhalifu wa kughushi na kuongeza muda wa noti hizi kukaa katika mzunguko kwa muda mrefu kabla ya kuchakaa, toleo hili limeongezewa ubora kwa kuweka alama maalum mpya za usalama na kutumia taaluma mpya ya kuziimarisha. Alama mbali mbali za usalama zimeboreshwa na kwa mara ya kwanza kabisa alama ya “motion” ambayo ni rahisi sana kutambulika kwa macho imetumika katika noti hizi. Ili kuelimisha wananchi kuhusu alama za usalama zinazotambulisha uhalali wa noti zetu, tumetoa matangazo na vipeperushi ambavyo vitasambazwa sehemu mbali mbali za nchi. Taarifa ya alama za usalama za noti pia zipo kwenye tovuti ya Benki Kuu kwa anwani www.bot-tz.org
Ni muhimu kwa umma kufahamu alama za usalama ili uweze kutofautisha noti halali na bandia kwa urahisi. Hata hivyo Benki Kuu inapenda kutahadharisha watu wawe waangalifu na kuzichunguza noti zote wanazopokea hasa kwenye giza ili kuhakikisha kwamba ni noti halali. Uchunguzi ufanywe kwa noti zote zilizopo kwenye mzunguko pamoja na za zamani. Endapo wana mashaka warejee kwenye mabango na vipeperushi vilivyotolewa na Benki Kuu au tawi lolote la Benki Kuu.
Gavana
Benki Kuu ya Tanzania
No comments:
Post a Comment