Hebu tafakari hizi nukuu za RAIS Jakaya Kikwete siku ya maadhimisho ya miaka 34 ya CCM huko Dodoma ambazo mimi nachukulia ni utetezi wake katika sakata la DOWANS.
"..Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka Tanesco ilipe..,"
“Wapo wanaosema niko kimya au nashindwa kuchukua hatua, kwa sababu marafiki zangu wamehusika. Nawalinda. Kwa sababu hiyo, nikaona nami nisema angalau watu wanisikie, lakini sina la ziada ni yale yale yaliyokwishasemwa”.
“Sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu viongozi wenzangu wameelezea kwa ufasaha uamuzi wa Kamati Kuu na ule wa kikao cha pamoja cha Wabunge wa CCM,”
“ Wapo waliosema lazima tulipe, wapo waliosema tusilipe, wapo waliosema tusiharakishe kulipa kwani kuna uwezekano wa kutokulipa kwa kutumia sheria,”
“ Uamuzi wangu ukawa tusiharakishe kulipa, tutafute njia za kuepuka katika kulipa. Ndiyo maana ya taarifa ya Chiligati na ile ya Waziri Mkuu,”
“ Tumewataka wanasheria wetu wasaidiane na wale wa Tanesco kuhakikisha hilo halitokei. Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka Tanesco ilipe,"
"Kauli za mimi kuhusika na Dowans inanishangaza, maana nisingeamua hivyo katika Kamati Kuu(CC) na Kamati ya Wabunge wa CCM. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi”
“ Sina hisa zozote wala manufaa yoyote yale, Pia sina ajizi wala kigugumizi cha kuchukua hatua kwa sababu ya rafiki yangu au hata kama angekuwa ndugu yangu kahusika. Maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu na Kamati ya Chama ya Wabunge wa CCM yalifanywa chini ya uongozi wangu,”
Ukifuatilia kauli hizo kuna kauli nyingi za Mhe Kikwete ambazo kama Rais hakustahili kuzisema, mojawapo ya ,ni kauli yake ya kwamba pamoja na kumsifu sana Nyerere lakini alishindwa kutatua changamoto nyingi katika utawala wake na hivyo hivyo kwa marais wengine waliomtangulia, sembuse mimi (Kikwete). Alisema hayo akijitetea kwamba yeye sio wa kwanza kushindwa kuondoa matatizo ya watanzania.
Huu ni utetezi RAHISI mno kwa jinsi alivyoshindwa kutatua matatizo ya watanzania. Sio tu Mhe.Kikwete ameshindwa kutatua matatizo bali ameyaongeza na kufanya maisha ya watanzania kuwa magumu zaidi. Mwl.Nyerere alijenga umoja wa kitaifa na alijenga uwajibikaji kwa watumishi wa umma kitu ambacho Kikwete ameshindwa. Mzee Ruksa aliruhusu uchumi wa soko ambao ulisaidi kufanya upatikanaji wa bidhaa muhimu ambazo mwanzo zilionekana kama anasa. Mzee Mkapa akajitahidi kujenga uchumi imara bila kusahau miundo mbinu na kurudisha heshima ya wafanyakazi. Pamoja na mapungufu yao viongozi waliopita wanayo ya kujivunia.
Kipindi hiki hakina umoja wa kitaifa, kuna makundi ndani ya CCM, matumizi makubwa serikalini, kuendekeza ununuaji wa magari ya kifahari yasiyo na tija, gharama za maisha zimepanda mno, thamani ya shilingi imeshuka sana, mfumuko wa bei hauelezeki, mitandao ya wizi mfano wizi wa EPA, mfumo wa elimu ni mbovu kwa kuanzisha kisiasa shule za kata zisizo na walimu wala vifaa nya kutosha hasa vya sayansi,
Mhe Kikwete amekiri na ameweka bayana Richmond ilikuwa kampuni ya mfukoni au Richmond in kampuni hewa. MASWALI: Kama hii ni kweli anatuambiaje kuhusu matokeo ya TAKUKURU waliosema kuwa Richmond haikuwa na shida? Kama ilikuwa kampuni hewa kwa nini aliruhusu ikauza mkataba na DOWANS na mkataba uleule ukatumika na Tanesco?
Je watendaji wenzake wa Serikali na CCM waliosema deni la Dowans halikwepeki walikuwa na maana gani kama yeye hataki deni lilipwe?
Je kama hakuona umuhimu wa kutoa tamko wakati watendaji wake wanatofautiana kauli, je ni nani aliyekuwa na kauli ya mwisho katika sakata hili?
Mimi ninaona nchi hii inahitaji sana mabadiriko ya namna ya kushughulikia masuala ya jamii.
No comments:
Post a Comment