Search This Blog

Tuesday, July 19, 2011

CHADEMA KUMCHUNGUZA SHIBUDA












CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeunda tume itakayoongozwa na Profesa Abdallah Safari kumhoji Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu zinazomkabili.

Hii ni mara ya pili kwa Shibuda kuhojiwa na jopo maalumu la Chadema kwani tayari aliwahi kuhojiwa baada ya kupingana na msimamo wa chama hicho wa kumsusia Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizundua Bunge Desemba mwaka jana kwa kuhudhuria dhifa katika Ikulu ya Chamwino huku akiweka bayana kupingana na msimamo huo.

Mapema mwezi huu alitoa tena kauli ambazo Chadema imeziita ni zenye kukiuka maadili hali iliyomfanya Mkurugenzi wake wa Mambo ya Nje, John Mnyika kuwasilisha malalamiko rasmi ndani ya Kamati Kuu (CC).

Akizungumza Dares Salaam jana baada ya kikao cha CC, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema hatua ya kuunda tume kwa ajili kufanya kazi ya kupitia tuhuma hizo imetokana na madai ya mlalamikaji kuwa na mantiki.

Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Edson Mbogoro, Said Mzee, Lazaro Masey na Ester Daffi ambaye si mjumbe wa kamati, bali atafanya kazi kama mratibu wa kamati hiyo akitokea Ofisi ya Katibu Mkuu.

Dk Slaa alisema: “Kikao cha kamati kilichokaa jana (Juzi) hakikujadili suala la Shibuda na mambo yaliyopo bungeni, bali kilipokea taarifa ya malalamiko kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu juu ya kitendo cha Shibuda kukiuka maadili. Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ili hatua ziweze kuchukuliwa kwanza ni lazima malalamiko yawasilishwe Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama naye kuyawasilisha kwenye Mkutano wa Kamati Kuu.”

No comments:

Post a Comment