Search This Blog

Friday, July 29, 2011

Msaada tutani....................
















JE ni Heri mbunge atolewe bungeni kwa kutetea nchi yake kama Wenje, Tundu Lisu, Mch Msigwa na Kamanda Lema kuliko mbuge yule anayelala bungeni kama Wassira  huku akisubiri kikao kiishe apokee posho ya 70,000''...????

MAJINA YA SHULE ZETU: ndo utamaduni?


Wednesday, July 27, 2011

Hili haliniingii akilini



















Jamani kuna watu wanapenda kuiga ubunifu wa wenzao. Walianza kuiga kwenye matumizi ya Helcopiter sasa wanaiga matumizi ya MAGWANDA!!! Mwishowe wataiga hata salamu.....utasikia ...Peoples powerrrrrrrrrrr!!!!!!!!!!!!

Tuesday, July 19, 2011

CHADEMA KUMCHUNGUZA SHIBUDA












CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeunda tume itakayoongozwa na Profesa Abdallah Safari kumhoji Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu zinazomkabili.

Hii ni mara ya pili kwa Shibuda kuhojiwa na jopo maalumu la Chadema kwani tayari aliwahi kuhojiwa baada ya kupingana na msimamo wa chama hicho wa kumsusia Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akizundua Bunge Desemba mwaka jana kwa kuhudhuria dhifa katika Ikulu ya Chamwino huku akiweka bayana kupingana na msimamo huo.

Mapema mwezi huu alitoa tena kauli ambazo Chadema imeziita ni zenye kukiuka maadili hali iliyomfanya Mkurugenzi wake wa Mambo ya Nje, John Mnyika kuwasilisha malalamiko rasmi ndani ya Kamati Kuu (CC).

Akizungumza Dares Salaam jana baada ya kikao cha CC, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa alisema hatua ya kuunda tume kwa ajili kufanya kazi ya kupitia tuhuma hizo imetokana na madai ya mlalamikaji kuwa na mantiki.

Wajumbe wengine wanaounda kamati hiyo ni Edson Mbogoro, Said Mzee, Lazaro Masey na Ester Daffi ambaye si mjumbe wa kamati, bali atafanya kazi kama mratibu wa kamati hiyo akitokea Ofisi ya Katibu Mkuu.

Dk Slaa alisema: “Kikao cha kamati kilichokaa jana (Juzi) hakikujadili suala la Shibuda na mambo yaliyopo bungeni, bali kilipokea taarifa ya malalamiko kutoka Ofisi ya Katibu Mkuu juu ya kitendo cha Shibuda kukiuka maadili. Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema ili hatua ziweze kuchukuliwa kwanza ni lazima malalamiko yawasilishwe Ofisi ya Katibu Mkuu wa chama naye kuyawasilisha kwenye Mkutano wa Kamati Kuu.”

MADUDU ALIYOFANYA KATIBU MKUU WA WIZARA YA MADINI NA NISHATI...HATIMAYE AJIUZURU RASMI LEO.

Katibu Mkuu wa wizara hiyo David Jairo (CHINI) amejiuzuru wadhifa wake leo baada ya wabunge kumjia juu kufuatia kitendo chake cha kuziandikia barua taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo zitoe mchango wa sh. milioni 50, ili kufaikisha mchakato wa kusomwa bajeti hiyo bungeni kama barua hiyo inavyosomeka hapo JUU.

Monday, July 18, 2011

WABUNGE WAKATAA UTITIRI WA MIPANGO YA NGEREJA!!!

Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini imekwama kupita na kusogezwa mbele kwa muda wa wiki tatu ili  kutoa majibu muafaka kuhusu mgao wa umeme pamoja na mambo mangine.
Hoja ya kuhairisha bajeti hiyo imetolewa na Kiongozi wa Serikali Bungeni Waziri mkuu Mizengo Pinda, bunge bila kujari itikadi za vyama limepitisha kwa kauli moja hoja hiyo.Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini mwaka 2011/12, ilikuwa mbaya na mbovu isiyofaa hata kupitishwa kwa kutoridhishwa na mipango iliyomo katika bajeti.Miradi 16 iliyohitaji Sh402.4 bilioni ikiwa ni pamoja na matumizi ya kawaida ni:-
1.     Mitambo ya kufua umeme ya megawati 100 jijini Dar es Salaam utakamilika Desemba mwaka huu
2.     Megawati 60 jijini Mwanza ambao utakamilika Juni mwakani.
3.     Kinyerezi (Dar es Salaam) wa megawati 240 (utakamilika mwaka 2013/14),
4.     Mnazi Bay (Mtwara) wa megawati 300 (utakamilika mwaka 2013/14),
5.     Somanga Fungu (Kilwa), megawati 230 (utakamilika mwaka 2013/14)
6.     Ruhudji, megawati 358 (utakamilika mwaka 2015/16).
7.     Mgodi wa makaa ya mawe Kiwira (Mbeya) megawati 200 (utakamilika mwaka 2013/14),
8.     Ngaka wa megawati 400 (utakamilika mwaka 2014/15),
9.     Mchuchuma megawati 600 (utakamilika mwaka 2014/15),
10.  Murongo/Kikagati (Kagerea) wa megawati 16 ambao utategemea kukamilika kwa makubaliano kati ya Serikali ya Uganda na Tanzania.
11.  Rusumo (Kagera) wa megawati 63 ambao upo kwenye taratibu za kutafutiwa fedha,
12.  Stiegler's Gorge (Pwani) wa megawati 2,100
13.  Mpanga wa megawati 165 (utakamilika mwaka 2015/16).
14.  Rumakali wa megawati 222 (utakamilika mwaka 2018),
15.  Dar es Salaam-Tanga ambayo ni ya dharura ikijumuiasha Symbion (megawati 112.5), Aggreko (megawati 100),
16.  Ununuzi wa mitambo itakayofungwa Majani Mapana, Tanga wa megawati 70 na ule wa gesi wa IPTL, Tegeta jijini Dar es Salaam.
Hebu tusubiri watakuja na mipango gani tena baada ya hizo wiki tatu!!!!

Wednesday, July 13, 2011

ROSTAM AJIVUA GAMBA:


HOTUBA YA MHE. ROSTAM AZIZ KWA WAZEE WA IGUNGA - TABORA
UTANGULIZI

WAZEE wangu, kwanza kabisa kabla ya kueleza kile ambacho kimenisukuma kuzungumza nanyi leo, napenda kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kufikia siku hii ambayo inatukutanisha waja wake.

Wazee wangu wa Igunga, baada ya kufanya hivyo napenda pia kutumia fursa hii kuwashukuru ninyi nyote mmoja mmoja na katika umoja wenu kwa kuitikia wito wangu, kijana wenu, niliyewaomba nije nizungumze nanyi siku hii ya leo.

Nafanya hivyo nikitambua vyema kwamba, kama si nyinyi wazee wangu na wengine wengi ambao hatuko nao hapa leo kwa sababu mbalimbali, ambao mmekuwa na imani kubwa nami nisingeweza kufikia hapa nilipofika sasa.

Wazee wangu, waasisi wa taifa letu walitufundisha kutambua na kuheshimu ukweli kwamba; ‘Uongozi ni Dhamana’ dhana ambayo kila ninapokaa na kutafakari huwa inanirejesha nyuma na kukumbuka jinsi nyinyi mlivyokaa katika umoja wenu na kuniteua mimi, miongoni mwa vijana wenu wengi, kuwa mwakilishi wa Jimbo la Igunga tangu mwaka 1994.

Katika kipindi hicho chote cha utumishi wangu, nyinyi wazee wangu mmekuwa mhimili muhimu ambao umeniwezesha kutimiza wajibu wangu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu nikitambua namna ambavyo mmekuwa na imani kubwa juu yangu.

Ari na moyo wa imani, ushirikiano na mshikamano ambao wazee wangu mmekuwa nao kwangu ndiyo ambao kwa kiwango kikubwa umetuwezesha kufanya kazi kwa pamoja, tukishinda changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikilikabili jimbo letu katika kipindi chote ambacho mmeendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.

Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

Miongoni mwa mafanikio makubwa tuliyoyafikia kupitia ushirikiano wetu na uongozi wa pamoja ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora lakini leo ndiyo ya kwanza, taa za barabarani, bima ya afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.

Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi chote ambacho mmendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa.

Wakati nikitambua na kuheshimu ukweli kwamba katika kipindi chote cha ubunge wangu mmekuwa na imani kubwa nami na kuniunga mkono kwa dhati, naamini kwamba kwa upande wangu pia nimejitahidi kwa kadiri nilivyoweza, kutimiza matarajio ya wananchi wa Igunga.

Wazee wangu, nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi hicho chote hayajaweza kumaliza changamoto zote za maendeleo ambazo zinatukabili.

Wazee wangu, ingawa nimekuwa na kawaida ya kukutana na kuzungumza nanyi mara kwa mara, mmoja mmoja na wakati mwingine katika umoja wenu, wito wangu wa leo una makusudi ambayo kwa kiwango kikubwa ni tofauti na yale ambayo tumeyazoea.

Japokuwa ujumbe ninaotaka kuzungumza nanyi wazee wangu, si mgeni sana masikioni mwenu, tofauti ya leo na mikutano yetu mingine iliyopita ni uamuzi ambao nimekusudia kuufanya na ambao nitayatangaza muda mfupi ujao.

YATOKANAYO

Wazee wangu, naamini mmekuwa mkifuatilia kwa karibu hali ya siasa nchini na hususani afya ya kisiasa na matukio mengine ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho mimi ni mwanachama wake na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) nikiuwakilisha Mkoa wetu wa Tabora.

Naamini kwamba katika kufuatilia kwenu mtakuwa mmebaini kuwapo kwa matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakitokea huku yakiligusa jina langu na wakati fulani nafasi yangu kama kiongozi wa chama hicho.

Wazee wangu, nayasema hayo kwa sababu mara kwa mara ninapokutana nanyi nikiwa katika ziara zangu jimboni na wakati mwingine mnapowasiliana nami kwa njia mbalimbali mmekuwa mkionesha kuguswa kushitushwa na kutaka kujua kulikoni kuhusu mambo hayo yanayotokea.

Mimi, kama mnavyonijua nyote, ni mtu muwazi na mkweli. Siku zote nimekuwa mwepesi sana wa kuwaeleza kuhusu kila kinachotokea ili kuwaondoa hofu na wakati huo huo kuwahakikishia kwamba masuala yasiyo na msingi hususani yale yanayogusa siasa za kitaifa hayawezi kutuondoa katika mstari sahihi wa kuwahudumia wananchi wa Igunga, mkiwamo nyinyi wazee wangu ambao mmeniamini na kunituma kuwawakilisha.

Nyinyi wenyewe ni mashahidi wazuri kwamba tangu matukio yanayogusa jina langu yaanze kutokea miezi michache tu baada ya Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikweti kuingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2005, tumekuwa tukiyapuuza na tukaendelea kufanya kazi pamoja kwa bidii.

Bado naamini na nitaendelea kuamini kwamba tulifanya uamuzi sahihi wa kuyapuuza matukio hayo kwani mbali ya kuendelea kutimiza malengo mbalimbali yaliyokuwamo katika Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM, pia mliendelea kuniamini kwa nafasi yangu ya kuwa mwakilishi wenu bungeni na hata mkaniruhusu nibebe jukumu jingine kubwa la kuwa Mjumbe wa NEC ninayewakilisha mkoa wetu wa kihistoria wa Tabora.

Wazee wangu, nyinyi ndiyo watu mnaolifahamu vyema jimbo letu la Igunga na hakika nyinyi ni sehemu muhimu ya watu wanaojua historia ya kisiasa ya Mkoa wa Tabora kwa miaka mingi hata kabla ya kuja kwa mfumo wa vyama vingi hapa nchini.

Hakuna shaka hata kidogo kwamba, Tabora ni kitovu hasa cha uasisi wa siasa za vyama vingi hapa nchini. Ni wazi kwamba huwezi ukazungumzia chimbuko la vyama vya upinzani tunavyoviona hapa nchini leo pasipo kugusa mkoa huu ambao umekuwa chimbuko la wanasiasa wenye mizizi hapa na nchini kwa ujumla.

Majina ya wanasiasa wa aina ya wazee wetu, hayati Chifu Said Abdallah Fundikira na Christopher Kassanga Tumbo, Kasela Bantu (Mungu awalaze mahala pema peponi), James Mapalala, Profesa Ibrahim Lipumba na mengi mengine yana mizizi yao katika Mkoa wetu wa Tabora.

Kutokana na ukweli huo basi ni wazi kwamba, nikiwa Mbunge wa Igunga kwa vipindi vinne mfululizo na wakati huo huo nikiwa Mjumbe wa NEC kwa vipindi vitatu mfululizo, moja ya kazi ambazo nimezifanya kwa uaminifu na kwa bidii kubwa huku nikiungwa mkono na kushirikiana nanyi ni ile ya kuhakikisha kwamba mkoa huu pamoja na kuwa kitovu cha upinzani unaendelea kubakia kuwa ngome muhimu ya kisiasa ya CCM.

Si vibaya tukakumbushana kwamba, wakati nachaguliwa kuwa mjumbe wa NEC wa Mkoa mwaka 1997, jimbo moja katika mkoa wetu lilikuwa likishikiliwa na upinzani. Leo hii Tabora ni mkoa pekee miongoni mwa mikoa iliyotuzunguka ambao haukupoteza jimbo hata moja kwenda upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2010. Mafanikio haya tuliyafikia kwa pamoja kutokana na ushirikiano wenu wazee wangu.

Wazee wangu, Waswahili wanasema usione vyaelea, vimeundwa. Kazi ya kuijenga CCM katika mazingira yenye mizizi hasa ya upinzani nikiwa mbunge na hususani M-NEC kutoka Mkoa wa Tabora haijapata kuwa rahisi na itaendelea kuwa ngumu na ambayo mapambano yake ni makali sana.

Wazee wangu, kwa namna ya pekee kabisa napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru nyinyi wazee wangu wa Igunga na wananchi wenzangu wote wa Mkoa wa Tabora kwa kushikamana na kuifanya kazi hiyo kwa bidii, uaminifu na mafanikio makubwa.

Matunda ya kazi hiyo kubwa yanaonekana. Pamoja na kuwa kitovu cha kihistoria cha siasa za upinzani, Tabora ndiyo mkoa pekee katika eneo hili ambao unaongozwa na wabunge wote kutoka CCM baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na hata kabla ya hapo.

Kwa sababu hiyo basi, wazee wangu, sote katika umoja wetu ukiacha mafanikio makubwa tuliyopata katika jimbo na Wilaya yetu ya Igunga, tunayo mambo mengine ya msingi ya kujivunia. Kwa moyo wa dhati na kwa unyenyekevu mkubwa napenda kuwapongeza kwa namna mlivyojitoa kukipigania na kukitetea chama chetu kwa ari na nguvu ya kipekee.

KUJIVUA GAMBA

Wazee wangu, chama chetu chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete kimeamua kwa kauli na nia moja kujitathmini na kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo yenye lengo la kukiwezesha kiendelee kubakia chama kinachoaminiwa na kuungwa mkono na Watanzania walio wengi.

Dhamira ya mwelekeo huo wa kufanya mabadiliko ya ndani ya chama chetu ilitangazwa rasmi na Mwenyekiti wetu Rais Kikwete wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM, mjini Dodoma.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Kikwete aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka na wanyama wengine kadhaa ya ‘Kujivua Gamba’.

Wazee wangu hatua ya kwanza ya utekelezaji wa azimio hilo na mwelekeo huo sahihi ilifanyika mjini Dodoma wakati wa kikao cha Kamati Kuu ya Taifa ya CCM ambacho mimi nilikuwa mjumbe wake.

Wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya chama chetu wa wakati huo kwa kauli moja tulikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa Mwenyekiti wetu fursa nzuri ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa Chama.

Wazee wangu, tulifanya hivyo tukionesha kuunga mkono kwa asilimia 100 kile ambacho bado naendelea kuamini kuwa ni mawazo sahihi na yenye mwelekeo thabiti ya Mwenyekiti wetu ambayo kwa kiwango kikubwa yalikuwa yakiakisi matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa urais, ubunge na udiwani wa Oktoba mwaka jana.

Niliseme kwa maneno machache tu hili. Ingawa ni kweli kwamba Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana umekirudisha madarakani chama chetu kwa kukipa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais, ubunge na udiwani kwa Tanzania Bara na Zanzibar, kiwango cha ushindi tulichopata kimeonyesha waziwazi dalili za wananchi kupunguza imani yao kwetu kuilinganisha na ilivyokuwa mwaka 2005.

Tungekuwa ni chama cha siasa cha ovyo iwapo tungepuuza kupungua kwa kura za rais kutoka zaidi ya asilimia 80 tulizopata mwaka 2005 hadi kufikia aislimia 61 mwaka jana kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 20 ya kura katika kipindi cha miaka mitano tu, hasa ikizingatia ukweli kwamba mgombea urais ni mtu yule yule.

Tungekuwa ni chama cha siasa kilichokosa umakini iwapo tungekaa pasipo kuchukua hatua zozote za kujiimarisha baada ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu kuonesha wazi kukua kwa upinzani ambao umeongeza idadi ya wabunge na madiwani katika pande zote mbili za muungano.

Matokeo hayo ya uchaguzi ambayo hapana shaka yamekitikisa chama chetu yalitukumbusha wasia ambao tuliachiwa na Baba wa Taifa aliyesema; ‘Bila ya CCM Madhubuti Nchi Yetu Itayumba’.

Wazee wangu, kwa sababu ya kutambua ukweli kwamba hakuna haki isiyo na wajibu kama nilivyosema awali, mimi na wenzangu tuliokuwa katika Kamati Kuu tuliona ulazima, haja na umuhimu wa kukubali kwa kauli moja wito wa kututaka tujiuzulu ikiwa ni hatua moja ya kujipanga na kukijenga upya chama chetu.

KUJIVUA GAMBA KWAPOTOSHWA

Wazee wangu, kilichotokea baada ya kujiuzulu kwetu kila aliye ndani na nje ya chama chetu amekisikia na anakifahamu. Chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wetu mpya, Mhe. Wilson Mukama, na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali.

Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu ambayo ilijiuzulu baadaye.

Mara tu baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ambayo naamini Mwenyekiti wetu aliianzisha kwa nia njema ilianza kuenezwa ikichukua tafsiri na mwelekeo tofauti na ule wa awali.

Wajumbe wawili wa Sekretarieti, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), Mhe. John Chiligati, na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Mhe. Nape Nnauye, walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini wale walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi vinginevyo watafukuzwa na chama.

Wazee wangu, baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC na ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi.

Baada ya awali kuwaeleza waandishi wa habari kwamba majina ya watuhumiwa hao yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada, mwishoni viongozi hao walikaririwa wakiyataja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo ambao walikuwa wakilengwa na maamuzi hayo.

Wazee wangu, nilishangazwa na kushitushwa na namna porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine tena baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini.

Niliseme hili mapema. Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa kwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu.

Pili, nilishangazwa na kushitushwa na hatua ya viongozi wa chama changu ambacho nimekitumikia kwa bidii na uaminifu mkubwa kufanya juhudi kubwa hata kukivisha kikao kitukufu cha NEC uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya kimakundi ya kisiasa yaliyo ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.

Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria ukiachilia mbali ushahidi wa wazi umeshathibitisha kwamba ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015.

Wazee wangu, nyinyi ni mashahidi kwamba, mbali ya mimi mwenyewe kujitokeza kupitia vyombo vya habari na kueleza wazi kwamba sijapata kujihusisha katika vitendo vyovyote vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au vya rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaonihusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa.

Wazee wangu, ni wazi kwamba kama chama chenye siasa chenye dhamana ya kuwaoongoza Watanzania kutoka katika lindi la ufukara, maradhi, matatizo ya makaazi na mengineyo siku zote tunapaswa kuwa makini katika kuhakikisha kwamba changamoto za kuwaongoza na kuwakomboa wananchi waliotupa dhamana hazitikiswi na mawimbi ya matakwa ya nyakati ama ya vyombo vya habari au wapinzani wetu wa kisiasa walio nje ya CCM.

Ni kwa sababu ya kulitambua hilo na hasa kuyatambua madhara yanayoweza kukipata chama chetu na nchi yetu iwapo tutaendekeza siasa za kupakana matope pasipo na sababu za msingi, kuchafuana kusikokoma na kulipizana kisasi ndiyo maana nimeona nitumie fursa hii kuzungumza nanyi wazee wangu ili kuweka kumbukumbu sahihi.

MAAMUZI YANGU

Wazee wangu, nimetafakari sana na kimsingi nimefikia hatua ya kupima yale ambayo yamekuwa yakisemwa na kuandikwa juu yangu na ambayo kwa mtazamo wangu unaoungwa mkono na wanafamilia yangu, marafiki zangu na washirika wangu wa kibiashara walio ndani na nje ya nchi, naona umefika wakati muafaka wa kuchukua hatua.

Kwa sababu ya kutambua uzito wa hatua ninazokusudia kuzichukua, niliona halitakuwa jambo la hekima hata kidogo iwapo ningefanya hivyo pahala pengine popote bali hapa Igunga mbele ya nyie wazee wangu.

Baada ya kukaa na wanafamilia yangu, marafiki na washirika wangu wa kibiashara niliona halitakuwa jambo la busara hata kidogo kuendelea kuvutana na viongozi wa chama changu na wanachama wenzangu wa CCM katika mambo ambayo yanaweza kumalizwa kwa njia muafaka.

Wazee wangu, sina budi niwaeleze kwamba, mbali ya athari za kisiasa na kifamilia, vita vya ovyo vya kisiasa kama hivi tunavyoviendesha na kuviendeleza ndani ya CCM na ndani ya nchi yetu huwa vina athari kubwa katika ulimwengu wa kibiashara. Athari kama hizo za kibiashara huingia ndani zaidi kuliko vichwa vya habari vya magazeti vinavyolenga kuchafuana, na athari hizo huwa kubwa zaidi kwa mtu kama mimi kwa sababu tofauti na wengine wengi hapa nchini, mimi ni mfanyabiashara wa kimataifa.

Katika ulimwengu wa kibiashara wa leo, vita hivi ambavyo vinaweza kuonekana kuwa ni vidogo tu vyenye malengo ya kuchafuana kisiasa, vinakuwa na athari kubwa katika uhusiano wa kibiashara kuliko hata wale wasioelewa wanavyoweza kukadiria. Ndiyo maana nimeona ni afadhali sasa niwape nafasi wale wanaoendesha siasa hizi uchwara na zisizo na tija waendelee na siasa zao hizo ambazo kwa bahati mbaya kwao, mimi sina muda nazo na siwezi kuwa sehemu yake. Na mimi kwa upande wangu niendelee na maisha yangu.

Kutokana na ukweli huo na sababu zote hizo basi, kwa moyo wa dhati na kwa nia thabiti, hatua ya kwanza niliyoiona kuwa ninapaswa kuichukua ilikuwa ni hii ya kuitikia wito unaotokana na msukumo wa ndani ya nafsi yangu wa kuamua kukomesha kabisa malumbano na mivutano isiyo na manufaa kwangu binafsi, kwa viongozi wa chama changu na chama chenyewe.

Msukumo huo si mwingine bali ni ule wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu nisingelikuwa nazo.

Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu.

Aidha, nimefikia uamuzi huo lengo likiwa ni kuwajengea heshima na imani machoni mwa wanachama na wananchi wengine, viongozi wangu ambao naamini baada ya mimi kujitoa watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili ambazo msingi wake ni dhamana kubwa walizo nazo za kukiongoza chama chetu na nchi yetu kupitia Serikali yake.

Wakati nachukua uamuzi huu, natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo.

Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, yatakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Kwa upande mwingine, uamuzi wangu huu naona ni fursa kwa viongozi wa Chama changu cha CCM kutafakari na kuamua njia wanayoiona wao ni sahihi kuichukua kwa hatima na mustakabali wa chama chetu na ambayo wanaamini itakipa nguvu mpya ya kisiasa dhidi ya vyama vya upinzani.

Sambamba na hilo, ninayo imani thabiti kwamba, uamuzi wangu wa kubakia kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM utakuwa chachu kwa chama changu na kwa Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi.

Mwisho kabisa, nikimalizia naomba nitumie fursa hii kutoa heshima za pekee kwa Rais Jakaya Kikwete kwa kazi kubwa aliyoifanyia na anayoendelea kuifanyia nchi yetu. Amefanya mengi na makubwa kuiendeleza nchi yetu na watu wake kuliko inavyothaminiwa na kufahamika. Kazi yake kubwa inashindwa kuthaminiwa na kufahamika kutokana na siasa chafu tunazoziendesha Tanzania. Wasia wangu kwa wanasiasa wenzangu, waandishi wa habari na Watanzania wenzangu kwa ujumla ni kuwa tunahitaji kuisaidia nchi yetu kwa kufanya siasa zenye mwelekeo wa kujenga ambazo ndiyo hasa zinapaswa kuwa siasa kwa maana halisi ya neno hilo.

Wazee wangu, baada ya maelezo hayo, nawashukuru sana kwa kunisikiliza na kunielewa.

Ahsanteni sana.

Mwisho…

Monday, July 11, 2011

UONGOZI MBOVU NDO UMESABABISHA HAYA:

Idadi ya vijana wasiokuwa na ajira inazidi kuongezeka, elimu katika mashule yetu inazidi kushuka. Huduma katika hospitali zetu na katika vituo vya afya ni mbaya kiasi cha watu kutumia mitishamba.
Sote tunajua kuwa maeneo mengi hapa nchini hawana chakula na watu wanaishi kwa mlo mmoja tu kwa siku, bei ya vyakula sokoni imepanda na thamani ya shilingi yetu imeshuka kuliko kipindi chochote kile tangu nchi hii ipate uhuru.

Uzalishaji viwandani umeshuka, na hakuna shirika la umma linalifanya vizuri, hakuna hata ndege kubwa ya serikali inayoruka. Aibu kubwa hii!!!
Kilimo kwanza ni wimbo uliotungwa, lakini hauna mchezaji wa wimbo huo. Hakuna ongezeko la mazao ya chakula na biashara ukiuliza unaambiwa ni ukame. Hivi wakati wanatunga huo wimbo hawakujua kuna ukame???

Giza!!!! Jamani Giza!!! Ni miaka takribani 50 ya uhuru wan chi hii nchi ni giza kila siku kwa mgao usioisha. Wakati huo viongozi wanazunguka duniani kutafuta wawekezaji. Je wawekezaji watawekeza gizani?
Kuna watanzania wameiba pesa za wananchi! Mafisadi wanatanua tu mitaani kama mabingwa wa ligi Fulani. Ukiuliza unajibiwa hakuna ushahidi wa kuwatia hatiani
Askari polisi kuuwa raia wasio na hatia imekuwa ni jambo la kawaida. Wamachinga wamepigwa risasi Mwanza lakini ikaonekana uchunguzi utafuata!! Wapi nyie mnaua watu?

SUGU ALONGA!

Jana tarehe 8 Julai 2011 Polisi walinikamata kwa kile walichokiita kuwa ni kufanya mkutano bila kibali.Hata hivyo, mtiririko wa matukio unaonyesha kwamba polisi walisukumwa na sababu nyingine kwa kuwa suala la taarifa kupelekwa polisi kama sheria zinavyohitaji lilishashughulikiwa na viongozi wa CHADEMA mkoa na wilaya ya Mbeya Mjini.
Leo tarehe 9 Julai 2011 pamoja na kutolewa kwa dhamana polisi wameonyesha nia ya kutaka kuzuia tamasha la wazi la bure ( ‘Burudani Nyumbani’) ambalo wasanii mbalimbali walikuwa walifanye kwa mwito wangu kwa ajili ya kutoa burudani na kuhamasisha maendeleo. Polisi wameonyesha vitendo vya kutaka leo kufanyike tamasha la fiesta pekee wakati ambapo matamasha haya yote mawili yameandaliwa na wadau tofauti katika maeneo tofauti.
Mpaka wakati huu ninapotoa taarifa hii wananchi wengi wamejikusanya katika uwanja wa Ruanda Nzovwe ambao ni maarufu kama Uwanja wa Dr Slaa wakisubiri tamasha hilo lakini polisi wameonyesha dhamira ya kutaka kuwatawanya.
Maneno na vitendo vya Jeshi la Polisi vinaelekea kuwa na uhusiano na kauli ambayo niliitoa hivi karibuni kupitia mtandao wa Facebook ya kutohitaji tamasha la Fiesta kufanyika Mbeya.Katika mazingira haya ni muhimu nikaeleza tu kuwa kauli yangu kuhusu Fiesta ilikuwa na madhumuni ya kuanzisha mjadala kuhusiana na suala zima la wizi na unyonyaji uliopo kwenye Sanaa, ambao sio tu unawanyima haki Wasanii, bali pia kukosesha mapato kwa Serikali ambayo yangetokana na kodi kupitia Sanaa ikiwemo muziki.
Nilifanya hivyo baada ya tamasha hilo kutangazwa kufanyika katika eneo ambalo wananchi wamenipa wajibu wa uongozi wa kuwatumikia na kuwawakilisha. Hivyo kwa niaba ya wananchi wa Mbeya Mjini wanaokosa mapato katika sanaa na wasanii wa Mbeya wanaokosa fursa kutokana na vikwazo nilichukua uamuzi wa kuwakilisha kupaza sauti kama ambavyo nimekuwa nikipaza sauti katika masuala mengine yanayogusa umma kama viwanda, kilimo, barabara za Mbeya Mjini na Haki za wanafunzi wa Elimu ya Juu pamoja na makundi mengine katika jamii.
Niliamua kupaza sauti katika hili kupitia Fiesta, kwa kuwa waandaji wake kimsingi ni sehemu ya vyanzo vya maovu kwenye maendeleo ya muziki hapa nchini. Fiesta ikiwa kitovu cha uonezi kwani hata Wasanii wanaoshiriki halipwi ipasavyo au hawalipwi kabisa. Na hii ni kutokana na wao kutumia njia haramu kuhodhi (monopolise)biashara ya muziki hapa nchini, huku wakiwanyima nafasi watanzania wengi kutumia vipaji na ubunifu wao kwenye biashara ya muziki.Waandaji wa Fiesta ndio wenye redio ya Clouds, Kampuni ya promotion ya Primetime, na pia wanahusika na N.G.O ya THT, waandaji wa matamasha ya injili, ikiwemo kuwa na ushirika katika Tamasha la Pasaka.Huku wakiwa na ushawishi wa hila kwenye Kili Music Awards (One Call Promotion) na mambo mengine yote muhimu yanayohusu Sanaa. Ikiwemo ujumbe wa bodi kwenye Tamasha la majahazi, Zanzibar. Lisingekuwa jambo baya kama wangetumia nafasi hizo kwa haki na maendeleo ya sanaa.

Kutokana na haya, kwa miaka mingi himaya (“empire”) hii imetumia nafasi yake dhalimu kukandamiza watu wengine hasa Wasanii. Kwa mfano kama Msanii hayupo kwenye hiyo “himaya” yao basi hana nafasi ya kutimiza ndoto yake. Na iwapo Msanii hakubaliani na taratibu zao au malipo finyu wanayowalipa Wasanii, basi watahakikisha wanampiga vita na hatimaye kuhujumu usanii wake ili atoweke, kwa kuwa tu hakubaliani nao. Msanii hana haki ya kufanya majadiliano ya kibiashara mbele yao. “Empire” hii imehodhi mpaka makampuni ya udhamini hapa nchini, ambapo makampuni haya yamekuwa magumu kutoa udhamini kwa wadau wengine kwa kuwa tu wao ni washirika wa “Empire” hii.
Walifikia hatua ya kuhodhi mpaka biashara ya usambazaji kwa “Wadosi” ambapo bila ya wao kuruhusu basi Msanii yeyote kazi yake haipewi nafasi ya kusambazwa wala kusikika. Hata kama nyimbo au album yake ni nzuri kwa kiasi gani.Kibaya zaidi wamehodhi mpaka nia njema ya Rais Kikwete katika kusaidia Sanaa na Wasanii. Mfano ni Studio ambayo Rais kupitia Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano alitangaza kuwa amewapa Wasanii wa Tanzania, lakini baadaye tukashangaa kusikia ipo mkononi! Pia Rais aliahidi na kutoa nyumba ya Serikali kwa Wasanii ambayo ingetumika kuendeshea Studio husika, lakini nyumba hiyo ya Serikali iliyotolewa na Rais sasa iko chini yao na ndio makao ya THT! Wamefanikiwa kumhadaa Rais kuwa wao ndio “Care takers” wa Sanaa ya Tanzania akawaamini na wao wanaitumia vibaya imani njema ya Rais kwao kufanya dhuluma.

Yote niliyoyataja juu, japokuwa hayo ni kwa uchache tu! Yanalalamikiwa sana na wasanii wengi na wadau hapa nchini, japokuwa wengi wameshindwa kujitokeza waziwazi kutoka na vitisho vya watu hawa. Vitendo hivyo wanavyofanya vimeleta madhara katika tasnia ya sanaa na matokeo yake ni kudumaa kwa maendeleo ya muziki hapa nchini. Vijana wengi wanaojihusisha na sanaa wamepoteza matumaini. Wengi walipata tegemeo la ajira kupitia muziki, lakini hali haipo hivyo tena. Vijana wengi wasanii wamekata tamaa kwa ajili ya ukandamizaji wa “empire” hii.
Na sio tu wasanii na wadau wengine wanawapoteza katika hili. Kwa watu hawa kuhodhi na kuvuruga kabisa biashara ya muziki, hata Serikali inapoteza fedha nyingi kupitia kodi. Kwa mujibu wa utafiti wa Dr. Jehovaness Aikaeli ambaye ni mchumi wa UDSM, hata katika hali hii mbaya ya biashara ya muziki, Serikali imepoteza Tsh. Milioni 18, kwa kutokusanya kodi kupitia muziki tu, ukiachilia mbali filamu na sanaa nyingine. Na iwapo hali itaboreshwa basi kodi hiyo itapanda mpaka wastani wa Tshs. Bilioni 50 kwa mwaka! Hizi sio pesa kidogo kwaserikali, hasa ukizingatia bajeti ya Wizara inayohusika na Utamadnuni ni Tsh bilioni 14, kwa mwaka, fedha ambazo mara nyingi hawapewi zote kutokana na Serikali kutokuwa na fedha ya kutosha! Lakini hapa utaona kukwa kodi ya mwaka peke yake ingetosha kwa bajeti ya Wizara na ziada kubwa ingebaki kwa miradi ya maendeleo kama kujenga Art Theatres n.k
Napenda ieleweke wazi kwamba mimi binafsi ni “Mhanga” au “victim” wa uharamia wa “himaya” hii kwa miaka mingi, tukupitia migogoro kadhaa ya kibiashara lakini kilichonisikuma kuchukua hatua hii; sio nafsi yangu pekee bali wajibu nilionao hivi sasa kama mwakilishi umma.Izingatiwe kuwa baada ya mimi kuchaguliwa kuwa Mbunge na wananchi wa Mbeya tena kwa kishindo, Serikali kupitia Wizara inayohusika na utamaduni na pia Baraza la Sanaa (BASATA), walinipongeza kwa barua huku wakinitaka niendelee na harakati za kupigania sanaa na wasanii kwa kutumia nafsi au jukwaa langu jipya Bungeni na nje ya Bunge. Jukumu ambalo nililikubali kwa mikono miwili kwani harakati za muziki huu si kitu kipya kwangu, ulianza kabla ya Ubunge na ndio ninachokifanya na hasa ukizingatia mimi pia sasa ni Waziri Kivuli (Shadow Minister) wa Wizara ya Habari, Vijana na Michezo.
Kwa lugha nyingine ujumbe nilioutoa wa kukataa Fiesta ni ishara ya mgomo wenye nia ya kutuma ujumbe wa madai ya msingi. Na historia inaonyesha kuwa, Wasanii wa Nigeria walianza kulipwa vizuri kama wanavyolipwa sasa baada ya kuanzisha migomo dhidi ya mapromota wanyonyaji wa nchini kwao.Na kama ni suala la kukuza uchumi na ajira, Ni nini mchango wa Fiesta na matamasha mengine kwa halmashauri za mji na majiji wanayopita na kuvuna mamilioni ya fedha kila siku?
Wenu katika kutaka haki,
Joseph Mbilinyi (Mb)
9/7/2011-Mbeya Mjini

Friday, July 8, 2011

VURUGU ZA WAMACHINGA NA POLISI: chanzo chajulikana........

Vurugu za wamachinga na mgambo zilizotokea juzi jijini hapa, zimedaiwa kusababishwa na mvutano baina ya ofisi ya Meya na Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza.

Madai hayo yalitolewa jana na Meya wa Jiji, Josephat Manyerere (Chadema), wakati akizungumza wa waandishi wa habari ambapo alidai kwamba ofisi yake haikupewa taarifa ya operesheni ya kuondoa wamachinga katika maeneo yasiyoruhusiwa kufanya biashara katika mtaa wa Makoroboi.

Alipofuatilia, alibaini kuwa hata ofisi ya Mbunge wa Nyamagana, haikuwa na taarifa ya operesheni hiyo, ambayo imesababisha watu saba kujeruhiwa na kwamba habari zilizoenezwa kuwa Chadema walihusika na vurugu hizo kwa sababu halmashauri
inayoongozwa na chama hicho ni ya uchochezi.


 Amesema kwa kuwa operesheni hiyo ni batili, amewataka wamachinga waendelee kufanya biashara katika maeneo ya Makoroboi, hadi suala lao litakapopelekwa kwenye Baraza la Madiwani, ili kutafutiwa utaratibu na maeneo yasiyo na bughudha. Mvutano huo wa kiuhusiano, umesababisha ofisi ya Mkurugenzi kutotoa ushirikiano kwa ofisi ya Meya na kutolea mfano wa uuzwaji wa viwanja katika eneo la Kiseke bila ofisi yake kujulishwa.

Aidha, ametoa wito kwa wamachinga kujitahidi kupanga bidhaa zao vizuri, ili watu wapate njia ya kupita na pia wasitumie vipaza sauti kutangaza bidhaa zao na kuhakikisha maeneo ya biashara yanabaki safi na wafanye biashara hizo kuanzia saa 10 jioni.

Amewaomba wenye misikiti na shule katika mtaa wa Makoroboi waendelee kuwavumilia hadi ufumbuzi wa kudumu utakapopatikana kutokana na kwamba kulegalega kwa uhusiano wa kikazi kumesababisha vurugu zilizotokea juzi.