Search This Blog

Friday, March 4, 2011

UKOSEFU WA MVUA...Mamlaka ya hali ya hewa mbona imekaa kimya????

Baadhi ya maeneo yanavyoonekana sasa kwa ukame.

HALI ya nchi yetu kiuchumi inaendelea kudorora kutokana na sababu nyingi, kubwa ikiwa ni ukosefu wa mvua. Kwa muda mrefu sasa Tanzania inapata mvua kidogo ikilinganishwa na miaka ya nyuma, hivyo kukwamisha maendeleo ya kilimo na kuliweka taifa katika hali tete ya chakula, ingawa Serikali inasema hali si mbaya sana.

Ukweli ni kwamba, hali si nzuri kiuchumi na chakula kutokana na kukosekana mvua za kutosha. Hata mvua za masika ambazo kwa kawaida zinaanza kunyesha mwezi Machi sehemu mbalimbali nchini, hazionyeshi dalili ya kuwepo kiasi cha kutosha mwaka huu.


Kinachotushangaza, Malamaka ya Hali ya Hewa imekaa kimya bila kutoa taarifa juu ya matarajio ya kuwepo kwa mvua za kutosha au la. Tunachojua ni kwamba, moja ya kazi ya Mamlaka ya Hali ya Hewa ni kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa nchini na kutoa taarifa kwa taifa ili kuiandaa Serikali na wananchi kuchukuhua tahadhari juu ya matukio yanayoweza kutokea kulingana na hali itakavyo kuwa.  

Kwa mfano, kama kutakuwa na mvua kidogo Serikali na taasisi nyingine za maendeleo ziandae mazingira ya kuwahamasisha wananchi kulima na kupanda mazao mapema na yale yanayostahimili ukame.  Kama mvua zikiwa nyingi ambazo zinatarajiwa kuleta madhara kama vile mafuriko, wananchi waweze kuandaliwa kuhamishia makazi yao sehemu za miinuko ili wasikumbwe maafa.

Kilimo cha Tanzania kinategemea mvua kwa aslimia 100 hivyo wananchi wanatakiwa kupewa taarifa za kuwepo kwa mvua au la, ili waweze kuandaa mashamba na kupanda mazao, au wasifanye hivyo. 


Kutokana ukimya wa mamlaka hiyo wakati huu tunapokabiliwa na matatizo mengi na hasa ya kukosekana kwa umme ambao kwa asilimia kubwa hutegemea mvua, tunajiuliza juu ya uwezo Mamlaka  wa kufanya kazi yake ipasavyo.  Mashaka yetu ni je, ina wataalumu wa kutosha na waliobobea katika fani hiyo? Kama wapo je, wanavifaa vya kutosha na vya kisasa kuweza kupata taarifa sahihi kama ilivyo katika nchi zilizoendelea? Kama havipo, Serikali imefanya nini, au haioni umuhimu wa mamlaka hii?

Katika nchi zilizoendelea idara, au mamlaka ya hali ya hewa inapewa umhumimu wa hali ya juu kwa sababu hakuna jambo linalofanyika katika sekta za kilimo, usafirishaji, biashara na maisha ya jamii bila kuwa na taarifa sahihi hali ya hewa. 
Umuhimu wa mvua katika nchi yetu unatambulika kwa sababu mfumo wetu wote wa uzalishaji unategemea maji ya mvua. Kwa mfano, umeme unaohitajika katika sekta za uzalishahi na huduma za jamii kama viwanda, miradi ya maendeleo, ujasiriamali, elimu, hospitali unategema nguvu ya maji ambayo chanzo chake ni kikuu ni mvua, ndiyo maana sasa hivi tuko gizani na huduma zote zimekwama.

Kilimo ambacho ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu kiko shakani, hivyo kuiweka nchi katika uwezekano wa kukumbwa na njaa kutokana na upungufu wa chakula ambao tayari umeanza kujitokeza katika maeneo kadhaa.

Tunasisitiza na kuimbusha Mamlaka ya Hali Hewa kufanya kazi yake ipasavyo na kulijulisha taifa juu matarijio ya mvua kuanzia sasa. Hofu yetu ni kwamba, kukaa kimya kwao kunaweza kuliingiza taifa katika matatizo makubwa ya kuanza kuchukua hatua za dharua badala ya kuandaa mikakati ya kukabiliana na majanga yanayoweza kusababishwa na kuwepo, au kutokuwepo kwa mvua.

No comments:

Post a Comment