MAREKANI INAHAHA KUBORESHA ELIMU YAKE....SISI WA-TZ TUMEJIPANGAJE?????
- Matokeo ya mtihani wa kimataifa yaliyotolewa hivi karibuni kwa wanafunzi wenye miaka 15 yamezua kizaazaa hapa Marekani. Katika matokeo hayo Marekani imeshika nafasi ya 17 katika kusoma, nafasi ya 31 katika hesabu na nafasi ya 23 katika sayansi. Alama ya jumla ya Marekani ikilinganishwa na nchi nyingi zilizoendelea ni "wastani" na kwa ujumla imefanya vibaya. Wanafunzi kutoka Korea ya Kusini, Finland, China, Singapore, Canada ndiyo wamefanya vizuri zaidi wakifuatiwa na nchi zinginezo. Wanafunzi kutoka mji wa Shanghai nchini China ndiyo wanaongoza kwa kupata alama za juu zaidi.
- Kwa Wamarekani jambo hili halikubaliki kwani wanajua kwamba bila kuwa nambari wani katika elimu, haiwezekani kwao kuendelea kuwa nambari wani kiuchumi na kitekinolojia ulimwenguni; na tayari wameshajiwekea malengo ya kurudi kileleni tena katika masomo yote ifikapo mwaka 2020. Wakiweza kufanya hivi, mahesabu yao yanaonyesha kwamba uchumi wao utaweza kujiongezea dola zipatazo trilioni 41 katika miaka 20 ijayo!
- Watawezaje kurudi kileleni? Hatua ya kwanza waliyoipendekeza ni kuimarisha taaluma ya ualimu na kuifanya iheshimiwe zaidi ili kuweza kuvutia wanafunzi wenye vipaji. Hii ni pamoja na kuwalipa walimu mishahara mizuri pamoja na marupurupu ya kutosha, kuwajengea mazingira mazuri ya kufanyia kazi na nafasi zinginezo za kujiendeleza. Ripoti hiyo inaonyesha kwamba katika nchi zinazofanya vizuri katika elimu, ualimu si kazi ya kiholela tu. Katika nchi kama Singapore, Finland na Korea ya Kusini, kwa mfano, ni wanafunzi bora pekee ndiyo huruhusiwa kujiunga na ualimu (bofya hapa). Hata katika nchi za Kiarabu mkakati kama huu tayari umeanza kupendekezwa.
- Nilishangaa kuona kwamba sisi tunafanya kinyume. Kimsingi wale wanaofeli ndiyo tunawabebesha jukumu la kuelimisha taifa huku tukiwalipa mishahara kidogo na kuwafanyisha kazi katika mazingira magumu sana hasa kule vijijini. Na hapa hatujawataja hawa wa"Voda Fasta!". Taaluma ya ualimu haiheshimiwi hata kidogo japo kusema kweli ndiyo mama wa kila taaluma na msingi wa kila taifa lililoelimika. Ndiyo maana kuna kipindi fulani walimu walitishia kugoma na waziri wa elimu wa wakati ule inasemekana alitoa tamko kwamba hata walimu wakigoma hakuna neno kwani anaweza kuokota watu mabarabarani na sokoni wakaingia madarasani kufundisha!Tutawezaje kuwa na elimu bora kama tunadharau taaluma ya ualimu namna hii? Ati, ni kwa nini hawa vijana wenye vipaji wanaopata divisheni wani tusiwape kila kitu ili wavutike na kwenda kusomea ualimu? Au tutakimbilia umasikini wetu na kusema kwamba hatuna pesa na kwamba programu ya aina hiyo haiwezekani?
- Jambo jingine lilinivutia katika ripoti hii ni hili. Karibu nchi zote zilizofanya vizuri sana zinatumia lugha yake zenyewe kufundishia madarasani. Wachina wana Kichina chao, Wakorea na Kikorea chao, Wafin wana Kifini chao n.k. Na sisi je? Tumeng'ang'ania sera ya lugha ambayo ni kichekesho, sera ambayo kimsingi haiwasaidii watoto wetu kumudu lugha yo yote kitaalamu kati ya zile tunazotumia. Kutokana na kizingiti hiki cha lugha, elimu yetu imebutuka na kuwa zoezi la kukariri tu hata kama hatuelewi hicho tunachokikariri kina maana gani. Hii kweli ni elimu?
- Kuna mengi ya kujifunza katika ripoti hii. Jambo la msingi ambalo inabidi tulitambue ni kwamba hatutaweza kuendelea bila kuwa na elimu bora inayowakaramsha vijana wetu na kuwafanya wawe tayari kwenda kupambana na dunia pale wanapomaliza masomo yao. Na kuboresha taaluma ya ualimu pamoja na kuwa na sera imara ya lugha ya kufundishia vinaweza kuwa mwanzo mzuri katika kuleta mabadiliko ya kweli katika mfumo wetu wa ualimu
No comments:
Post a Comment