LICHA ya Mganda Davis Ntare kutwaa taji la Tusker Project Fame 2010, jopo la majaji kwa pamoja na uongozi wa chuo cha mafunzo cha shindano hilo wamekiri kwamba mshiriki wa Tanzania, Peter Msechu, ana kila sababu ya kuwa ndiye mshindi wa shindano.
Kila mtu kwa wakati wake, majaji Ian, Hermes Joachim na Juliana Kanyomozi, walimtaja Msechu kuwa ni mwanamuzikii maarufu anayejiamini sana na kujiweza jukwaani, na pia mbunifu.
Sifa hizo ndizo zinazotakiwa kwa mwanamuziki wa karne hii iliyojaa utandawazi, walieleza majaji.
Msechu ambaye kete yake ya mwisho aliitupa kwa kutumia kwa kibao cha Kilwa Jazz aliudhihirishia tena umma wa wengi katika Afrika Mashariki kwamba anaweza kuwainua kwenye viti na kuwaimbisha muda wowote anaotaka.
Msechu, huku akionyesha kujiamini kwamba muziki ni njia pekee ya kueleza hisia zake kwa jaji huyu kwani, angepata wapi nafasi nyingine ya kumwambia.
"Ningemuita nikamwambia nina maongezi naye angekuja?", alisema Msechu katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya onyesho hilo kwisha na washindi kutajwa katika maeneo ya Ruaraka, jijini Nairobi, eneo ambapopia yapo makao makuu ya East African Breweries, watengenezaji wa bia ya Tusker.
Akizungumza na Mwananchi, Msechu ambaye ameshinda mkataba wa mwaka mmoja wa wa kurekodi na Kampuni ya Africa Sound yenye makao makuu nchini Kenya alisema anaamini kuwa yeye ni mshindi, ila zawadi kubwa amechukua Davis, na atalithibitisha hilo atakapoanza rasmi kazi yake ya muziki, mashabiki wataendelea kufurahi kumsikiliza na kumuona jukwaani.