Search This Blog

Monday, April 23, 2012

SAINI ZIMETIMIA!!!!!!!!!!


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
HOJA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU BUNGENI KWA MUJIBU WA KATIBA
IBARA YA 53A NA KANUNI YA BUNGE, KIFUNGU CHA 133 KUWASILISHWA KWA
SPIKA KESHO TAREHE 23/04/2012


• Masharti yametimizwa; wabunge 73 wazalendo wamesaini
• Ni mwendelezo wa ‘Operesheni Uwajibikaji’


Mnamo tarehe 19/04/2012 wakati nahitimisha hoja ya Kamati ya Bunge ya
Mashirika ya Umma nilieleza kusudio langu la kuwaomba waheshimiwa
wabunge waniunge mkono katika kutia saini zisizopungua asilimia 20 ya
wabunge wote ili kuweza kutimiza matakwa ya Katiba ibara ya 53A kwa
ajili ya kuwasilisha Bungeni hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu.
Mnamo tarehe 20/04/2012 niliandaa orodha ya waheshimiwa wabunge wote
na kuisambaza ndani na nje ya ukumbi wa Bunge ili waheshimiwa wabunge
wote waweze kutia saini hizo, na mpaka leo tarehe 22/04/2012 orodha
hiyo imetimiza idadi ya wabunge wazalendo wanaopigania uwajibikaji 73
kutoka vyama vyote vyenye uwakilishi Bungeni, isipokuwa chama cha UDP
ambacho kina Mbunge 1 na hajatia saini waraka huo mpaka sasa.
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge kifungu cha 133 (1) kinasomeka “Mbunge
yeyote anaweza kutoa taarifa ya maandishi kwa Spika ya kutaka kuleta
hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa ibara ya 53A ya
Katiba” na kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (3) kinasomeka “hoja ya
kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu haitajadiliwa na Bunge
isipokuwa tu kama;


(a) “taarifa ya maandishi iliyowekwa saini na kuungwa mkono na Wabunge
wasiopungua asilimia 20 ya wabunge wote itatolewa kwa Spika, siku
zisizopungua kumi na nne kabla ya siku inayokusudiwa kuwasilishwa
Bungeni;”


Hali kadhalika kanuni za Bunge Kifungu cha 133 (4) kinasomeka kuwa
“hoja inayotolewa chini ya Kanuni hii na iliyotimiza masharti ya
Katiba,itawasilishwa Bungeni mapema iwezekanavyo na itaamuliwa kwa
kura za siri”.


Hivyo basi baada ya kutimiza matakwa ya kikatiba na kanuni za Bunge
kesho tarehe 23/04/2012 tutawasilisha rasmi kwa Spika Taarifa ya
Maandishi kwa mujibu wa kanuni 133 (1) na (3) ya hoja ya kutokuwa na
imani na Waziri Mkuu kwa kushindwa kusimamia uwajibikaji wa Serikali
Bungeni kwa mujibu wa ibara ya 52 na hivyo kulinda Mawaziri wenye
kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na kulisababishia hasara
taifa.


Tunatarajia kwamba siku kumi na nne baada ya kuwasilisha hoja hiyo
Bunge litakutana kwa haraka kujadili hoja hiyo ili kuwezesha
uwajibikaji na hatua kuchukuliwa za kuhakikisha mapendekezo ya ripoti
za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na maazimio ya Bunge
yanatekelezwa. Hoja hii ni mwendelezo wa ‘Operesheni Uwajibikaji’
hivyo tunaomba wabunge wazalendo na watanzania wote waiunge mkono ili
kuimarisha Uwajibikaji wa Viongozi, kupambana na ubadhirifu na
kunusuru uchumi wa nchi na kuchangia katika ustawi wa wananchi.
Kwa niaba ya wabunge wazalendo waliotia saini kuunga mkono taarifa ya
hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu ni;

…………………………….
Kabwe Zuber Zitto.
Mbunge Jimbo la Kigoma Kaskazini.
22/04/2012.

No comments:

Post a Comment