Search This Blog

Sunday, February 19, 2012

Dr. Mwakyembe amjibu DCI Manumba

Dk. Harrison G. Mwakyembe (Mb), NW-UJ
Dar es Salaam
18/02/12
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nimelazimika leo Jumamosi, tarehe 18 Februari, 2012 kutoa taarifa hii kwa vyombo vya habari kufuatia mkutano wa DCI Robert Manumba na waandishi wa habari jana (17/02/12) kuongelea, pamoja na mambo mengine, hali yangu ya afya na kuhitimisha, kienyejienyeji tu kuwa “sikunyweshwa sumu” ila naumwa tu ugonjwa wa ngozi bila kufafanua ugonjwa huo wa ngozi umesababishwa na nini!
Napenda nisisitize mapema kabisa kuwa msimamo huo wa Jeshi la Polisi umenikera sana katika hali niliyonayo ya ugonjwa, kwanza kwa kuingilia mchakato wa matibabu yangu na uchunguzi wa kina kuhusu kiini chake unaoendelea hospitali ya Apollo nchini India ambako bado sijahitimisha matibabu yangu; pili kwa ufinyu wa uelewa unaojitokeza bayana kwenye tamko la Jeshi la Polisi unaosisitiza kuwa “sikunyweshwa sumu” wakati sumu si lazima unyweshwe ili ikudhuru, inaweza kudhuru hata kwa kugusishwa tu; na tatu kwa Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye suala ambalo kwa takriban mwaka mzima halijawahi kuwa na dhamira ya dhati ya kulielewa au kulichunguza mbali na kulifanyia mzaha kupitia magazetini.
Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Februari, 2011 nilimwandikia barua IGP Said Mwema kumtaarifu kuhusu njama za kuondoa maisha yangu na ya viongozi wengine. Kwa kutambua kuwa Jeshi la Polisi la Tanzania daima husisitiza kuletewa ushahidi kwanza ndipo lifanyekazi, nilihakikisha nimeainisha katika barua  hiyo kila ushahidi nilioupata au kupewa. (Utaratibu huu wa Jeshi la Polisi kusubiri kuletewa ushahidi mezani, kama ambavyo mahakimu wanavyosubiri ushahidi mahakamani, haupo popote pale duniani (ila Tanzania tu) kwani kazi ya msingi ya Polisi si kuletewa, ni kutafuta ushahidi. Polisi wanachohitaji duniani kote ni kupata clue au tetesi tu. Hiyo inatosha kufukua ushahidi wote unaohitajika). Pamoja na kujitahidi kuanika kila aina ya ushahidi niliokuwa nao, mambo manne yalijitokeza ambayo yalionyesha wazi kuwa Polisi hawakuwa na dhamira ya dhati ya kupeleleza suala hilo:
(i)                Siku chache baada ya kumkabidhi IGP barua hiyo, nilitumiwa timu ya “wapelelezi” ofisini kwangu kuja kuchukua maelezo yangu ya ziada. Timu hiyo ilikuwa inaongozwa na ACP Mkumbo, afisa wa polisi ambaye wiki chache zilizokuwa zimepita alikuwa miongoni mwa askari waliotuhumiwa kupokea rushwa kwa lengo la kumbambikizia madawa ya kulevya mtoto wa Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, suala ambalo mpaka leo hii uongozi wa Polisi umeshindwa kulitolea maelezo ya kuridhisha. Kwa msingi huo, nilikuwa nimeletewa mtuhumiwa wa rushwa/ ujambazi kuendesha uchunguzi wa watuhumiwa wengine wa ujambazi! Nikatambua mara moja kuwa zoezi zima lilikuwa la mzaha, tena mzaha mkubwa!
(ii)              Wiki chache baada ya barua yangu kuwasilishwa kwa IGP na timu ya ACP Mkumbo “kuanza kazi”, Jeshi la Polisi likachukua hatua ya kuwapongeza na kuwazawadia askari niliowatuhumu kushirikiana na majambazi! Huhitaji kuwa profesa wa falsafa kuelewa kuwa huo ulikuwa ujumbe tosha wa kunipuuza.
(iii)            Hivi karibuni tuhuma za askari polisi kujihusisha na vitendo vya ujambazi mkoani Morogoro zilipopamba moto na kuwagusa askari “wale wale” niliowatuhumu kwenye barua yangu, IGP alichukua hatua ya kuwahamishia mikoa mingine!
(iv)           ili kunikatisha tamaa kabisa, barua yangu ya “siri” kwa IGP ikavujishwa kwa makusudi kwenye vyombo vya habari na kuchapishwa kama habari ambayo ilikebehi na kukanusha taarifa nzima niliyotoa, sijui kwa faida ya nani! Lakini huu ni mchezo wa kawaida kwa polisi kwani hivi karibuni Mhe. Waziri Samuel Sitta alipohojiwa na ofisa mwandamizi wa Jeshi la Polisi ofisini kwake, wakiwa wawili tu, taarifa ya kikao hicho ikawa kwenye moja ya magazeti ya mafisadi ikikebehi ushahidi aliotoa Sitta! The integrity of the police force leadership is on the line.
Nimeelezea vizuri katika barua yangu kwa IGP kuwa kundi hilo la mauaji lilikuwa limeelekezwa kuniua kwa kutumia sumu, taarifa ambayo kwa karibu mwaka mzima Polisi hawakutaka kuifuatilia kwa sababu wanazozijua wenyewe.  Sasa huu msukumo mpya wa Jeshi la Polisi kutaka kujua kama nilipewa sumu au la na kukurupuka kutoa tamko hata kabla ya kunichunguza nilivyo, kunihoji mimi na wasaidizi wangu ofisini na hata kuongea na mabingwa wa Kihindi wanaonifanyia uchunguzi, umetokea wapi?  Si ni polisi hawahawa ambao, badala ya kushukuru,  wamekuwa wakikerwa na tahadhari ambazo Waziri Sitta amekuwa akitoa ili suala hili lichunguzwe kwa kina?
Aidha napata taabu kuamini kama DCI Manumba na wenzake waliisoma taarifa halisi ya matatibabu yangu au walisoma taarifa “nyingine”, na kama waliisoma taarifa hiyo wenyewe au “walisomewa”! Nasema hivyo kwa kuwa alichokisema DCI Manumba kwa wandishi wa habari hakifanani kabisa na picha iliyo kwenye taarifa halisi ya Apollo ambayo inatamka wazi kuwa kuna kitu kwenye bone marrow kinachochochea hali niliyonayo, kitu ambacho mabingwa wanahangaikia kukijua, kukidhibiti /kukiondoa huku vyombo vyetu vya dola vikipelekeshwa na mafisadi kusema bila msingi wa kisayansi wala aibu: “hakulishwa sumu”, “hakulishwa sumu”!
Nimesoma darasa moja Kitivo cha Sheria Mlimani na DCI Manumba. Baadaye IGP Mwema alikuwa mwanafunzi wangu wa sheria Mlimani. Vigogo hawa wawili wa usalama wa raia nchini hawajanitendea haki, nao wanajua. Wanajua vilevile kuwa sitakaa kimya au kumung’unya maneno come what may pale ambapo haki inakanyagwa.
Tuendelee kuombeana afya na uhai ili tutendeane haki na vilevile tuitendee nchi yetu haki kwa kuvimalizia viporo vinavyokera vya Dowans, EPA, Kagoda n.k. kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
 
Mungu Ibariki Tanzania .

Monday, February 13, 2012

Zambia wameiduwaza dunia:


Zambia imechukua ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika 2012 baada ya kuwafunga Ivory Coast kwa mikwaju ya penati 7-8.
Mchezo huo ulimaliza dakika 90 za kawaida, kabla ya kwenda muda wa ziada, na hadi katika mikwaju ya penati.
Ivory Coast wamekosa penati 2 kati ya walizopiga ambapo Kolo Toure na Gervinho walikosa mikwaju hiyo.
Ivory Coast wataendelea kusubiri kunyakua kombe hilo, licha ya kuwa na wachezaji kadhaa wanaocheza Ulaya hasa katika Ligi Kuu ya England.
Tembo wa Ivory Coast walipoteza katika mchezo wa fainali mwaka 2006 dhidi ya Misri kwa mikwaju ya penati.
Lakini kwa Chipolopolo, ambao wamewahi kushika nafasi ya pili mara mbili, wamemaliza kwa ushindi kwa kuhanikizwa na vifo vya wachezaji wenzao mwaka 1993, baada ya ndege yao kuanguka karibu na uwanja ilipochezewa fainali mjini Libreville.
Mara ya mwisho kwa timu hiyo kutoka Kusini mwa Afrika kufika fainali ilikuwa mwaka 1994, mwaka mmoja tu baada ya wachezaji 18 wa nchi hiyo kupata ajali ya ndege karibu na mji mkuu wa Gabon.
Wakielekea katika mchezo wa fainali, wachezaji hao wa sasa walisema wanahisi nguvu kutokana na kukumbuka janga lililowapata wenzao.
Kwa kushinda mchezo wa fainali, wameonesha dhamira ya kuwashinda wapinzani wao ambao walikuwa wakipewa nafasi kubwa ya kupata ushindi.

Usalama barabarani TZ

Kwa mtindo huu ajali hazitaisha. lakini ukumbuke Trafic wapo kila mahali. Je hawalioni hili? Tafakari

Friday, February 10, 2012

CHADEMA WASABABISHA MAREKEBISHO YA SHERIA YA KATIBA

Tutakuwa hatutendi haki kama hatutasimama kama Watanzania kutoa pongezi za dhati kabisa kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kwa kusimamia kidete suala la Katiba mpya mpaka sasa marekebisho ya sheria ya Katiba mpya yakapitishwa na bunge leo.Ni wazi watu mbalimbali akiwemo Rais Kikwete wamechangia hili lakini bila kumung’unya maneno niseme kama si CHADEMA kusingekuwa na hoja hii ya Katiba mpya leo.

Kwanini?

· CHADEMA iliweka suala la Katiba mpya kwenye ilani yake ya Uchaguzi mwaka 2010
· Wabunge wa CHADEMA walitoka nje ya bunge siku Rais alipolifungua bunge pamoja na mambo mengine kudai katiba mpya itakayotoa fursa ya kuwa na tume huru ya uchaguzi
· Mwaka mzima wa 2011 CHADEMA iliongoza maandamano nchi nzima kutoa elimu ya uraia na kutaka kuungwa mkono na UMMA juu ya kupata katiba mpya
· Wabunge wa CHADEMA walitoka nje ya bunge mwezi Novemba 2011 kupinga mswada wa Katiba mpya uliokuwa na Mapungufu mengi na ya kimsingi
· Kamati kuu ya CHADEMA ilinyoosha Mkono wa mapatano na serikali kwa kukutana na Rais Kikwete kupinga mswada uliokuwa mbovu uliopitishwa kiushabiki na wabubge wa CCM na CUF
· Rais aliridhia mapendeklezo yote ya CHADEMA na kuamuru mabadiliko ya sheria iliyokuwa imepitishwa kishabiki na wabubge wa CCM na CUF
· Hatimaye marekebisho ya sheria yakapitishwa na bunge na kufungua rasmi mlango wa kutengeneza katiba mpya ya Tanzania.

Ni wazi kwa yote yaliyotajwa hapo juu yanatufanya tuamini CHADEMA imesimama imara katika kupigania Katiba ya nchi.Watanzania wengi walikata tamaa na kudhani baada ya mswada mbovu kupitishwa mwaka jana CHADEMA ingesusia moja kwa moja zoezi zima.Lakini CHADEMA imejenga taswira tofauti kwa Watanzania kwa kupigana kwa hali yoyote kuhakikisha Katiba mpya inapatikana.

Wafuatao wanastahili heshima ya pekee:

Pamoja na CHADEMA kama taasisi kuonekana kukomaa na kusimamia agenda zake,ni lazima tuwatambue baadhi ya watu walioongoza mpambano huu kwa Amani na utulivu na siku moja wataingia katika vitabu vya historia
· Dr Wilbroad P. Slaa-Ni kiongozi makini,madhubuti na anayeweza kuyasimamia maneno yake kwa kuinadi ilani ya CHADEMA nchi nzima wakati wa kugombea urais mwaka 2010 na watu wakaamini na kuona umuhimu wa Katiba mpya.Lakini Pia ni Katibu mkuu ambaye ni mtendaji mkuu wa chama anayeongoza sekretariati ya chama inayopanga agenda za chama na kusimamia mikakati yote ya chama,suala la Katiba mpya likiwa mojawapo ya mkakati.
· Freeman A.Mbowe-Huyu ni kiongozi wa upinzani bungeni na muda wote ameiongoza vema kambi ya upinzani bungeni kusimamia agenda hii ya katiba mpya.Hakutetereka na amekuwa akisimamia uwajibikaji wa pamoja wa kambi yake bungeni.Kwa jinsi leo alivyohitimisha mswada huu wa katiba mpya hawezi kusahaulika kirahisi.Amewafanya watanzania sasa kutambua ni nini maana ya kambi ya upinzani bungeni.
· Zitto Z.Kabwe-Huyu ni Naibu kiongozi wa upinzani bungeni na siku zote amekuwa msaidizi muhimu na wa kuaminiwa wa kiongozi wa upinzani bungeni.Ni wazi amesaidia sana kuifanya kambi ya upinzani kuwa kama jinsi ilivyo na anastahili kufurahia matunda ya kupigania katiba mpya ndani ya bunge.
· Tundu A.Lissu-Ni mnadhimu mkuu wa upinzani bungeni.Huyu ukitaja jina lake kwa sasa hata mtoto mdogo anamjua.Hili ni jembe kweli kweli.Alipinga kwa nguvu zote mswada mbovu wa mwaka jana.Kutokana na upinzani wake kwa mswada wabunge wa CCM na CUF walimshambulia kwa kila neno baya ili kumchafua mbele ya jamii.Lakini alisimama kidete kupambana ndani na nje ya bunge mpaka leo hii walau watanzania wanafurahia mabadiliko ya sheria ile.
· Wabunge wote wa CHADEMA-Hawa kwa ujumla wao wamesimama kidete kwa umoja ndani na nje ya bunge kuhakikisha katiba mpya inapatikana.Kila walichokifanya kuhusu katiba ni msimamo wa chama chao.Wote walinena lugha moja.Hakika huu ni mfano wa kuigwa kwa vyama vingie pale kunapokuwa na jambo la msingi la kuwatetea watanzania.Iliwashangaza wengi pale hata mbunge wa Maswa John Shibuda alipoungana na wenzake mwaka jana kutoka nje ya bunge kususia mswada mbovu uliowasilishwa.
  • Rais Jakaya Kikwete-Kwa heshima ya Pekee anastahili pongezi za dhati kabisa kwa uamuzi wake wa kukubali mwito wa kukaa na CHADEMA.Ni wazi Rais alikubali kuweka pembeni itikadi ya chama chake na kuamua kuwasikiliza CHADEMA na hatimaye kuyakubali madai yao yote.Ilihitaji moyo mkuu kufanya hivi.Aliipuuza kelele za wana CCM wenzake waliokuwa hawataki akubaliane na CHADEMA.Aliwapuuza na kuwadharau wabunge wa chama chake waliotishia kupiga kura ya kutokuwa na Imani na Rais kisa eti amekubali mapendekezo ya CHADEMA ili kupata katiba bora kwa Taifa letu.Wana CCM wengine wakadiriki kusema Rais anafanya haya kwa vile anamaliza muda wake wa urais kwa hiyo anajiandalia mwisho mwema,lakini hata hawa pia Rais aliwapuuza kwa maslahi ya Katiba bora.Kwa hili hakika Jakaya Kikwete amejiandikia historia ambayo haitafutika kirahisi.
Kwa ufupi kabisa niseme waliyoyafanya CHADEMA yameingia kwenye historia mpya.Yatasimuliwa vizazi na vizazivijavyo na ni mfano kwa wanasiasa na vyama vingine vyote.Hakika wameonyesha ukomavu wa hali ya juu.Na labda niseme lakini msiniite mtabiri! Kwamba ikipatikana Katiba mpya ya watu,ambayo itatoa tume huru kabisa ya uchaguzi itakayotenda haki kwa vyama vyote mwaka 2015,basi watanzania msishangae kumuona Michael Satta wa Tanzania akimrithi Jakaya Kikwete.Na tusubiri tuone.

Mungu awatangulie watanzania katika kupata katiba bora mpya ya Tanzania.Alilolipanga Mungu mwanadamu kamwe hawezi kulipangua.

CHANZO: jamii forum: by fmpiganaji;

Hali tete Muhimbiri

Hapa Viti vya wagonjwa vinarudishwa ndani

Mgonjwa amelala chini

Mgonjwa anarudishwa nyumbani

Mgonjwa anaandaliwa kurudishwa nyumbani baada ya hali kuwa mbaya hospitalini