Search This Blog

Wednesday, August 31, 2011

KIZUNGUMKUTI CHA VITAMBULISHO VYA TAIFA.


Mchakato wa Vitambulisho vya Taifa umeanza tangu mwaka 2007 (kama sikosei). Ni baada ya Baraza la Mawaziri kuubariki Februari 2 mwaka huo. Mwaka 2012 mchakato huu utatimiza miaka mitano. Unagharimu Shilingi bilioni 222! Hiki ni kioja !
Maana; mpaka mradi huu uje ukamilike, basi, yumkini kuna watanzania ambao watakuwa wameshakufa hata bila kuvikamata hivyo vitambulisho vyenyewe. Na pia tujiulize; katika hali yetu ya sasa, mradi wa vitambulisho vya kitaifa unakwamishwa na nini? Kwa hali hii kama wananchi walio wengi wangeambiwa wachague leo, kati ya kitambulisho na nafuu ya bei ya mafuta na sukari, basi, haraka wangechagua kuwepo kwa unafuu wa mafuta na sukari.

Ni tangu enzi za Waziri Joseph Mungai, akaja Lawrence Masha, na sasa Vuai Nahodha. Kila mmoja anakuja na lwake! Bunge la Bajeti 2009 yalisemwa haya na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha:“Naomba kuwathibitishia Watanzania kupitia Bunge lako tukufu kwamba, mradi wa vitambulisho utakamilika kwa kufuata sheria na utaratibu, bila mizengwe, kwa uwazi unaostahili na bila upendeleo,”
Akasimama mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, (CCM) na kusema kwa jazba;“Kama waziri mwenyewe hajui kinachoendelea katika wizara yake ina maana hakuna kinachoendelea. Halafu anatuambia mchakato unaendelea, mchakato gani huo?” aliuliza Shelukindo.
Naibu Spika Anne Makinda akasimama na kutamka: “Mheshimiwa waziri na mheshimiwa mbunge, hapa tunasikilizwa na wananchi nchi nzima. Wanachotaka kujua ni je; vitambulisho watavipata au hawatavipata? Hilo ndilo wanalohitaji na sio kuna nini”.
Waziri Masha akasimama na kusema; ” Mheshimiwa Naibu Spika, vitambulisho vitapatikana ndani ya mwaka huu wa fedha 2009/2010.”
Naam, mpaka hii leo ni August 2011 hakuna cha kitambulisho cha kitaifa wala nini! Waziri Masha alituongopea Watanzania, na hajawahi kutuomba radhi na hayuko tena bungeni. Nani wa kutuomba radhi kwa uongo huu wa serikali ya CCM?????

Serikali iwe wazi kama kuna tatizo la utekelezaji wa mradi wa vitambulisho vya taifa lieleweke ili wadau waweze kutoa maoni mazuri ya uharakishaji wa utekelezaji huo.
Nawasilisha.

No comments:

Post a Comment